Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Italia na Afrika wamekubaliana kukuza na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali hasa zile za biashara na uwekezaji, lengo likiwa ni kuleta maendeleo barani Afrika.
Mawaziri hao wamefikia makubaliano hayo wakati wa mkutano wa pili wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa Italia na Afrika uliofanyika katika mji wa Farnesina, -Italia na kuhudhuriwa na mawaziri kutoka zaidi ya nchi arobaini akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dkt Augustine Mahiga.
Mawaziri hao walikutana kwa lengo la kujadili kwa pamoja changamoto zinazohusu usalama, uhuru, amani, demokrasia na namna wadau wa Italia watakavyoweza kushiriki katika kukuza uchumi barani Afrika hasa katika sekta ya uwekezaji na biashara.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliofunguliwa na Rais wa Italia, -Sergio Mattarella, Waziri Mahiga amesisitiza suala la amani na kuongeza kuwa ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi Barani Afrika.
Pamoja na kuhudhuria mkutano huo, Waziri Mahiga pia alipata fursa ya kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, – Enzo Moavero na Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), – Gilbert Houngbo.
Katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia wamekubaliana kuandaliwe hati ya makubaliano kati ya Tanzania na Italia ya kufanya majadiliano ya mara kwa mara yenye lengo la kukuza ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, elimu na utamaduni.
Balozi Mahiga amesema kuwa katika mazungumzo yake na Rais huyo wa IFAD wamekubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Mfuko huo kwenye maeneo makuu manne ambayo ni huduma za kifedha kwa wakulima wadogo, kuwajengea uwezo vijana ili waweze kufanya kilimo kama sehemu ya ajira, kuboresha sekta ya mifugo pamoja na masuala ya lishe bora.
Houngbo amemuahidi Waziri Mahiga kuwa IFAD itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye miradi inayoendelea ikiwemo ile ya programu ya miundombinu ya masoko, uongezaji wa thamani na kuwawezesha wakulima wadogo wa vijijini kifedha.