Iran yakiri kuiangusha ndege ya Ukraine

0
252

Jeshi la Iran limekiri kuwa liliilenga kwa kombora kimakosa ndege ya abiria ya Ukraine baada ya ndege hiyo kupita kwenye eneo nyeti la Jeshi la Kimapinduzi la Iran.

Taarifa imeeleza kuwa jambo hilo lilitokea kwa makosa ya kibinadamu huku serikali ikiahidi kuwashughililia watu wote waliohusika.

Awali Iran ilikanusha kudungua ndege hiyo Januari 8 mwaka huu jijini Tehran na kupelekea vifo vya watu wote 176.

Lakini imekiri kufanya hivyo kufuatia Marekani na Canada kusema kuwa taarifa za kiintelijensia zinaonesha kuwa Iran iliilenga kwa kombora ndege hiyo, pengine kwa bahati mbaya.

Ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Canada kupitia Ukraine ilianguka karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Imam Khomeini muda mfupi baada ya kuanza safari.