Iran imethibitisha kuwa itatumia mashine za kisasa zaidi kurutubisha madini yake ya Urani katika awamu ya Tatu ya kujiondoa kwenye mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 kati yake na Mataifa yenye nguvu Duniani.
Msemaji wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Iran, – Behrouz Kamalvandi amewaambia Waandishi wa habari kuwa, licha ya nchi hiyo kujiondoa polepole katika mkataba huo, bado itaruhusu Jumuiya ya Kimataifa kufuatilia kazi zake.
Tangazo hilo la Shirika la Nguvu za Atomiki la Iran, litaipa nafasi nchi hiyo kuharakisha mchakato wa urutubishaji wa madini hayo ya Urani kwa kiwango cha asilimia Ishirini.
Wakati hayo yakiendelea, Kaimu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki ( IAEA ) Cornel Feruta amewasili nchini Iran hii leo kwa lengo la kukutana na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo ili kujadili suala hilo.