Iran kuendelea kujiimarisha Kijeshi

0
1106

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema kuwa nchi yake itaendelea kujiimarisha kijeshi na kuendeleza mpango wake wa silaha za nyuklia licha ya shinikizo kutoka kwa nchi alizozitaja kuwa mahasimu zinazotaka kudhibiti uwezo wake wa kujihami.

Rouhani ametoa kauli hiyo wakati akiwahutubia maelfu ya raia wa Iran wakati wa maadhimisho ya miaka 40 tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Amesisitiza kuwa Iran haijamuomba mtu ama Taifa lolote na wala haitaomba ruhusa ya kutengeneza aina mbalimbali ya makombora na itaendelea na mkakati wake wa kujiongezea nguvu za kijeshi ili kujihami zaidi.

Mamilioni ya raia wa Iran na watu kutoka mataifa mbalimbali wanahudhuria maadhimisho hayo ya miaka 40 tangu mapinduzi ya Kiislamu katika mji mkuu wa Iran – Tehran na miji mingine ya nchi hiyo.

Maadhimisho hayo yanachukuliwa kama ushindi wa mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa Kifalme Februari 11 mwaka 1979 nchini Iran.