Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai -ICC imetengua hukumu dhidi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Jean-Pierre Bemba, kwa makosa ya uhalifu wa kivita yaliyofanywa na jeshi lake binafsi katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Bemba alihukumiwa kifungo cha miaka 18 mwaka 2016 baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kuwaamuru wapiganaji wake kwenda kutekeleza mauaji katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati Oktoba 2002 na kuanzisha mapinduzi dhidi ya Rais wa wakati huo Ange-Felix Patasse.
Hata hivyo katika uamuzi uliotolewa hii leo Jaji amesema Bemba hawezi kuwajibishwa kwa makosa yaliyofanywa na wapiganaji wa jeshi.
Jaji huyo Christine Van den Wijngaert amesema majaji katika hukumu iliyotolewa mwaka 2016 walishindwa kuzingatia jitihada zilizofanywa na Bemba kusitisha vitendo vya uhalifu baada ya kupatiwa taarifa.