Homa ya dengue yaitesa Singapore

0
155

Nchi ya Singapore imekumbwa na mlipuko wa homa ya dengue inayoambukizwa na mbu weusi wenye madoadoa ya kung’aa wajulikanao kama Aedes na kuathiri idadi kubwa ya watu.

Zaidi ya watu elfu 11 wameripotiwa kuambukizwa homa hiyo katika kipindi cha kuanzia mwaka huu hadi hivi sasa, ambapo mwaka 2021 kipindi kama hicho watu 5,258 waliugua ugonjwa huo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Singapore, Desmond Tan ametangaza hali ya tahadhari na kusema kuwa homa hiyo inaenea kwa kasi kubwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duñiani (WHO), kwa sasa ugonjwa huo umeenea kwa zaidi ya nchi 100.

Ripoti ya WHO ya mwezi Januari mwaka huu imebainisha kuwa idadi ya watu wanaougua homa ya dengue imeongezeka mara 30 katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Dalili za homa ya dengue huanza kuonekana ndani ya siku tatu hadi 14 mara baada ya kuambukizwa ikiwa ni pamoja na homa, kuumwa viungo vya mwili na inapozidi husababisha kutokwa na damu hata kifo.