Hofu miongoni mwa Watangazaji yasababisha Kituo cha Redio kufungwa

0
703

Kituo kimoja cha Redio ya Kijamii katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), ambacho kimekua kikifanya jitihada kubwa za kuhamasisha jamii namna ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola kimefungwa, baada ya Mtangazaji wake mmoja kuuawa.

Baadhi ya Watangazaji wa kituo hicho cha Redio cha Lwemba kilichopo kwenye mji Mambasa Mashariki mwa DRC wamesema kuwa, mara kwa mara wamekuwa wakipokea vitisho vya kutaka kuuawa na kwamba wameamua kusitisha matangazo kwa sababu za kiusalama.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Papy Mumbere Mahamba ambaye ni mmoja wa Watangazajj wa kituo hicho cha Redio, aliuawa nyumbani kwake saa chache baada ya kutoka kufanya kipindi kinachowahimiza Raia wa DRC kuungana ili kupambana na ugonjwa wa Ebola, ambao tayari umesababisha vifo vya watu wengi katika Jamhuri hiyo

Zaidi ya watu Elfu Mbili na Mia Mbili wamefariki Dunia katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo baada ya kuugua Ebola, tangu ugonjwa huo ulipozuka katika Jamhuri hiyo mwaka 2018.

Hofu ya kuuawa imetanda miongoni mwa Wafanyakazi wa Afya katika mji huo wa Mambasa, hasa kwa Wafanyakazi ambao wamekua wakitoa elimu kwa Jamii ya namna ya kujikinga na Ebola ili ugonjwa huo usiendelee kuenea.