Ghorofa laanguka nchini Kenya

0
629

Ghorofa moja linalotumika kwa ajili ya makazi ya watu limeanguka katika eneo la Tassia jijini Nairobi nchini Kenya.

Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu kuanguka kwa jengo hilo, lakini inahofiwa kuwa huenda kuna watu wamefunikwa na kifusi cha jengo hilo.

Picha mbalimbali ambazo zimekua zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zimeonyesha watu kadhaa wakitolewa kwenye vifusi.

Baadhi ya watu walioshuhudia tukio la kuanguka kwa jengo hilo wamesema kuwa, watu watatu wameokolewa baada ya jengo hilo kuanguka na wameshuhudia wakipelekwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Hadi sasa haijafahamika ni watu wangapi bado wamenasa kwenye kifusi cha jengo hilo ama ni watu wangapi waliofariki dunia katika tukio hilo.

Sababu za kuanguka kwa jengo hilo hazijafahamika, lakini imekua ni kawaida kwa majengo yaliyojengwa chini ya viwango nchini Kenya kuanguka baada ya kunyesha kwa mvua kubwa.