Watu 30 wamethibitika kufariki dunia katika ghasia zinazoendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini Afrika Kusini.
Ghasia hizo zinaendelea huku kukiwa na maandamano yaliyodumu kwa takribani wiki moja, kupinga hatua ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kufungwa miezi 15 gerezani.
Habari kutoka nchini Afrika Kusini zinaeleza kuwa hali ni mbaya zaidi katika jimbo la KwaZulu – Natal, ambako ni nyumbani kwa Zuma.
Polisi nchini Afrika Kusini wamewakamata zaidi ya watu 800 kufuatia ghasia na maandamano hayo, ghasia ambazo pia zimegubikwa na uharibifu wa mali na uporaji.
Akilihutubia Taifa, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema ghasia zinazoendelea nchini humo hivi sasa hazijawahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.
Tayari Rais Ramaphosa ameamuru vikosi vya Jeshi la nchi hiyo kupelekwa katika maeneo mbalimbali kuwasaidia Polisi kukabiliana na waandamanaji.