Ghasia zazuka Anjouan

0
2165

Wakazi wa kisiwa cha Anjouan nchini Comoro wamesema kuwa kumekuwa na milio ya risasi katika mitaa ya mji mkuu wa kisiwa hicho wa Mutsamudu baada ya vikosi vya ulinzi na usalama kuondoa vizuizi barabarani vinavyodaiwa kuwekwa na wafuasi wa upinzani.

Wizara ya Mambo ya Ndani   ya Comoro imewashutumu waandamanaji wa upande huo wa upinzani kwa kutumia silaha za moto na kusema kuwa madai kuwa vikosi vya serikali vimefyatua risasi hayana ukweli wowote.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa Gavana wa kisiwa cha Anjouan, – Abdou Salami Abdou ambaye ni mwanachama wa upinzani ndiye aliyepanga maandamano na ghasia katika mji mkuu wa Mutsamudu.

Kumekuwa na maandamano pamoja na ghasia katika kisiwa hicho  cha Anjouan chenye mkusanyiko wa visiwa vingi katika bahari ya Hindi tangu  mwezi Julai mwaka huu,  baada ya Rais Azali Assoumani kushinda kura ya maoni yenye utata na kumaliza utamaduni wa kuongoza kwa mzunguko na kumfanya aendelee kukaa madarakani.