FIFA KUCHUNGUZA SALT BAE ALIVYOINGIA UWANJANI?

0
149

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) linachunguza jinsi mpishi maarufu “Salt Bae”ambaye jina lake halisi ni Nusret Gökçe, alivyoingia uwanjani baada ya fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar.

Mpishi huyo wa Uturuki, ambaye anamiliki msururu wa migahawa yake ya Nusr-Et katika miji ya London, Dubai na New York, alionekana akiwa amelishika, kulibusu na kujifanya ananyunyiza chumvi kwenye Kombe la Dunia akisherekea na wachezaji wa Argentina baada ya ushindi wao dhidi ya Ufaransa.

Sheria za FIFA zinaelekeza kombe hilo linaruhusiwa kuguswa au kushikiliwa na kundi la watu maalum waliochaguliwa wakiwemo washindi wa mashindano na maofisa wa FIFA.

Umaarufu wa Salt Bae ulipatikana kupitia mitandao ya kijamii mwaka wa 2017 baada ya video iliyosambaa mitandaoni ikionyesha mbinu yake ya kuandaa na kuonja nyama mbele ya wateja wake wakati wa chakula cha jioni.

David Beckham, Leonardo DiCaprio na Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, ni miongoni mwa wadau wake wanaojulikana kutembelea mgahawa wake na kujipatia chakula hapo.