Fedha za ujenzi wa ukuta zaanza kutolewa

0
462

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeidhinisha malipo ya Dola Bilioni Moja za Kimarekani zitakazolipwa kwa  Wahandisi wa jeshi la nchi hiyo kwa ajili ya ujenzi wa ukuta  katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Fedha hizo ambazo ni za awali, zitatumika kujenga ukuta huo wenye uzio wa kilomita 91.

Habari zaidi zinasema kuwa fedha  hizo ni sehemu ya Dola Bilioni 5.7 za Kimarekani  zilizotangazwa na Rais Donald Trump wa Marekani  Februari 15 mwaka huu, kutolewa kama dharula kwa ajili ya ujenzi huo.

Kwa kutangaza hali ya dharula kwa ajili ya ujenzi wa ukuta huo, Trump alipata uwezo wa kutolihusisha Bunge la nchi hiyo ili kuidhinisha fedha hizo na hivyo kujenga ukuta kwa kutumia fedha za Jeshi.

Rais Trump amesisitiza kuwa ni lazima kuwepo kwa ukuta katika eneo la mpaka wa Marekani na Mexico ili kuzuia vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na watu ambao wamekua wakivuka mpaka na kuingia nchini humo.