Viongozi wa Umoja wa Ulaya (EU) wanaokutana mjini Brussels nchini Ubelgiji wamekubaliana kuendeleza vikwazo vya uchumi dhidi ya Russia kwa muda wa miezi Sita zaidi.
Vikwazo hivyo viliwekwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014 baada ya Russia kuliteka jimbo la Crimea ambalo ni sehemu ya mashariki ya Ukraine.
Vikwazo hivyo vilivyotarajiwa kuondolewa mwezi Januari mwaka 2020, lakini baada ya kuongezwa kwa muda huo sasa vitaendelea kutekelezwa hadi mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huo wa 2020.
Wachunguzi wa masuala ya kiuchumi wamesema kuwa, hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya kuendeleza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Russia itaathiri sekta mbalimbali nchini humo zikiwemo zile za Nishati, Fedha na Jeshi.
Hata hivyo Umoja wa Ulaya umesema kuwa, vikwazo hivyo vitalegezwa endapo mkataba wa kusimamisha mapigano uliotiwa saini mjini Minsk baina ya Russia na Ukraine mwaka 2015 utatekelezwa.