Erdogan atoa maelezo kuhusu mauaji ya Khashoggi

0
1994

Rais Recep Tayyip Erdogan  wa Uturuki ametoa maelezo ya kwanza rasmi juu ya mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul na kudai kuwa mauaji hayo yalipangwa.

Rais Erdogan amesema kuwa mpango wa mauaji hayo ulianza kuandaliwa Septemba 29 mwaka huu na kwamba aliuawa Oktoba pili.

Amesema kuwa kamera za ubalozini hapo ziliondolewa kabla ya mauaji hayo na siku moja kabla ya mauaji wataalamu wa uchunguzi wa jinai waliwasili mjini Istanbul na baada ya Khashoggi kuuawa mmoja wa wataalamu hao alivaa nguo zake na kutoka ubalozini hapo ili aonekane kuwa mwandishi huyo alitoka.

Rais Erdogan ameutaka utawala wa kifalme wa  Saudi Arabia uwataje wote waliohusika na mauaji ya Khashoggi ambao pia walirekodi kila kitu kilichofanyika.

Rais huyo wa Uturuki ametaka watuhumiwa 18 waliokamatwa nchini Saudi Arabia kwa kuhusika na mauaji hayo wapelekwe nchini Uturuki kujibu mashtaka yao na kuongeza kuwa  hana mashaka na uadilifu wa mfalme wa Saudi Arabia lakini anachotaka ni uchunguzi wa uwazi.