Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Kenya (COTU) umeitaka serikali kuzipiga marufuku kampuni zote ambazo zimekuwa zikiwatafutia ajira raia wa nchi hiyo huko Saudi Arabia.
COTU imetoa kauli hiyo baada ya kusambaa kwa video ikimuonesha mwanamke mmoja wa Kenya aliyepelekwa kufanya kazi nchini Saudi Arabia akinyonyesha mbwa.
Katibu Mtendaji wa COTU Francis Atwoli amesema mwanamke huyo aliondoka nchini Kenya akiwa ameacha mtoto mchanga mwenye umri wa miezi miwili na alipofika Saudi Arabia mwajiri wake alimlazimisha kunyonyesha mbwa.
Atwoli ameiomba serikali kuchukua hatua kama zilizowahi kuchukuliwa na Rais wa zamani wa Taifa hilo Hayati Mwai Kibaki ambaye alipiga marufuku kampuni zote zinazofanya kazi ya kuwatafutia ajira raia wa Kenya nje ya nchi.
Raia wengi wa Kenya hasa vijana wamekuwa wakienda nchini Saudi Arabia kutafuta ajira kwa madai ya kutokuwepo kwa ajira za kutosha nchini humo na wakiwa huko wamekuwa wakifanya kazi za nyumbani na vibarua.
Hata hivyo wakifika nchini humo, wengi wao wamebainika kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.