China na Japan zimekubaliana kuimarisha uhusiano wa kiuchumi katika kipindi hiki ambapo China iko kwenye mzozo wa kibiashara na Marekani.
Hayo yamebainika wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi hizo mbili wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Japan, – Shinzo Abe nchini China.
Waziri Mkuu huyo wa Japan akiwa na mwenyeji wake ambaye ni Waziri Mkuu wa China, -Li Keqiang amewaambia waandishi wa habari nchini China kuwa masuala mengine waliyokubaliana ni pamoja na kushirikiana ili kuondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea Kaskazini.
Maeneo mengine ni katika teknolojia ya kisasa, ulinzi wa haki miliki na biashara ya kubadilisha sarafu katika nyakati zinapotokea dharura za kifedha.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa China, – Li Keqiang amesema kuwa nchi hizo ni majirani muhimu na kwamba amani, urafiki na ushirikiano ni masuala ya msingi kwa pande zote.
Hiyo ni ziara ya kwanza kufanywa na Waziri Mkuu wa Japan nchini China katika kipindi cha miaka saba.