China na Ethiopia zimesitisha usafiri wa ndege kwa kutumia ndege aina ya Boeing 737 Max 8.
Hatua hiyo inafuatia ndege ya aina hiyo mali ya Shirika la Ndege la Ethiopia kuanguka katika mji wa Bishoftu nchini humo na kuua watu wote 157 waliokuwamo ndani, ambao ni abiria 149 na wafanyakazi Wanane.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya China imesema kuwa usafiri kwa kutumia ndege za aina ya Boeing 737 Max 8 utaendelea kusitishwa mpaka hapo kitakapobainika chanzo za ndege za aina hiyo kupata ajali za mara kwa mara.
Kwa sasa kampuni kubwa ya uundaji ndege ya Boeing ya nchini Marekani inafanya utafiti kufuatia ndege hiyo mali ya kampuni ya Ndege ya Ethiopia kuanguka zikiwa zimepita dakika sita tu tangu iruke kutoka mjini Addis Ababa, – Ethiopia na ilikua ikielekea Nairobi nchini Kenya.
Hiyo ni ndege ya pili kuanguka ndani ya kipindi cha miezi mitano ikihusisha muundo wa Boeing 737 Max 8, ambapo mwezi Oktoba mwaka 2018 ndege ya aina hiyo ilianguka nchini Indonesia.
Swali kubwa ambalo kampuni hiyo ya Boeing inajiuliza ni je ndege za aina hiyo zina matatizo ya kiufundi, kwani zimekua zikipata matatizo licha ya kuwa ni mpya.