Bunge la Tanzania limewasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano wa 52 wa Jukwaa la Kibunge la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF) wakati wa Mkutano wa 53 unaoendelea jijini Arusha.
Taarifa hiyo imewasilishwa leo na mjumbe wa Bunge hilo Selemani Zedi, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Kibunge la nchi za SADC, kwa niaba ya Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson.
Akiwasilisha ripoti hiyo kuhusu Usawa wa Kijinsia, Maendeleo ya Wanawake na Vijana, Seleman Zedi amesema, Bunge kwa kushirikiana na Serikali limefanikiwa kutunga Sheria mbalimbali zinazolinda haki za wanawake hususani za umiliki wa mali na uwezeshaji kiuchumi.
Amebainisha kuwa Serikali imeandaa mpango wa kuanzisha vitalu vya kilimo vilivyowekwa mifumo ya umwagiliaji kwa jamii ili kujenga kesho bora (BBT) pamoja na kuchimba visima visivyopungua 10 katika kila wilaya kwa lengo la kuwezesha kilimo cha umwagiliaji na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Kuhusu Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Zedi ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania ipo kwenye mkakati kabambe wa kuondoa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hususani wa mipakani ili kuchochea maendeleo katika maeneo hayo.
Katika Mkutano huo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linawakilishwa na Wajumbe watano ambao Seleman Zedi, Shally Raymond, Hawa Mwaifunga, Dkt. Alfred Kimea na Kassim Haji.