Rais George Weah wa Liberia amewaomba Wabunge wa Bunge la nchi hiyo
kukatisha likizo yao na kukutana kwa dharura kujadili mambo muhimu
yanayolihusu Taifa hilo likiwemo lile linaloelezwa kuwa ni ukosefu wa fedha.
Taarifa iliyotolewa na Bunge la Liberia haijatoa taarifa zaidi kuhusu ombi hilo, lakini habari zisizo rasmi zinaeleza kuwa huenda Rais Weah anataka kuliomba Bunge kuidhinisha uchapishwaji wa Dola Bilioni 35 za nchi hiyo kwa ajili ya kulipa mishahara ya Watumishi wa Serikali katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu za mwisho wa mwaka.
Liberia imekumbwa tatizo la ukosefu wa fedha na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa Wabunge na Watumishi wa Serikali, ambao wamekua wakilalamikia kitendo cha kucheleweshewa mishahara yao ya kila mwezi.