Brazil yakamata mali za Teodorin Obiang

0
2200

Serikali ya Brazil imekamata fedha taslimu pamoja na saa za thamani, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 16 za Kimarekani kutoka kwa watu waliofuatana na Makamu wa Rais wa Equatorial Guinea, – Teodorin Nguema Obiang.

Obiang mwenye umri wa miaka 48 anafahamika kama ni mtu ambaye amekua akiishi maisha ya kifahari na ni mtoto wa rais wa nchi hiyo ya Equatorial Guinea yenye utajiri mkubwa wa mafuta, -Teodoro Obiang Nguema.

Sheria za Brazil haziruhusu mgeni yeyote kuingia nchini humo akiwa na zaidi ya dola elfu mbili na mia nne za kimarekani kama fedha taslimu.

Rais Teodoro Obiang Nguema wa Equatorial Guinea ambaye ni kiongozi wa Afrika aliyekaa madarakani kwa muda mrefu na mtoto wake wamekua wakituhumiwa kwa kutumia vibaya mapato ya fedha za mafuta, huku asilimia 70 ya raia wa nchi hiyo wakiishi katika hali ya umaskini.

Watu 11 waliofuatana na Teodorin Nguema Obiang wamesafiri kwa ndege ya serikali ambapo polisi nchini Brazil wamekuta kiasi hicho cha  fedha pamoja na saa za thamani kwenye mabegi tofauti.