Bouteflika kutowania tena Urais

0
500

Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amesema kuwa hatawania tena kiti hicho kwa muhula mwingine wa Tano.

Katika taarifa yake Rais  Bouteflika  aliyeiongoza Algeria kwa muda wa miaka Ishirini amesema kuwa kipaumbele chake kwa sasa ni kuangalia hali ya afya yake na kuhakikisha raia wa nchi hiyo wanapata uongozi sahihi.

Bouteflika amekua akionekana hadharani mara chache na hata kushindwa kutekeleza majukumu kadhaa ya Urais tangu mwaka 2013 alipopata maradhi ya kiharusi.

Uchaguzi wa Rais nchini Algeria ulipangwa kufanyika Aprili 18 mwaka huu, lakini hata hivyo nao umeahirishwa huku Baraza la Mawaziri nalo likitarajiwa kuvunjwa muda wowote kuanzia hivi sasa.

Tayari Waziri Mkuu wa Algeria, -Ahmed Ouyahia ametangaza kujiuzulu wadhifa huo na nafasi yake imechukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo  Noureddine Bedoui ambaye atakua na jukumu kubwa la kuunda Baraza jipya la Mawaziri.

Kumekua na maandamano katika miji mbalimbali nchini Algeria ambapo Raia wa nchi hiyo wanapinga hatua ya Rais Bouteflika kutaka kuwania muhula wa Tano wa uongozi.