Bill Gates kupambana na nzige waliovamia Afrika Mashariki

0
501
Nzige wamevamia nchi sita za Afrika Mashariki na wana uwezo wa kula chakula sawa na watakachokula watu 35,000 kwa siku moja wakiwa kwenye eneo la kilomita 1 ya mraba, FAO imeeleza.

Taasisi ya Bill & Melinda Gates imechangia dola za kimarekani milioni 10 (Tsh 23.1 bilioni) kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na nzige wavamizi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mchango huo utakabidhiwa kwa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) la Umoja wa Mataifa (UN) ambalo limekuwa likiwasihi watu na taasisi mbalimbali kuchangia fedha kukabiliana na nzige wanaohofiwa kusababisha njaa kutokana na kuvamia mazao.

Katika salamu zake za shukrani, Mkurugenzi Mtendaji wa FAO, QU Dongyu amesema hadi sasa UN imekusanya shilingi bilioni 76 za kitanzania, huku lengo likiwa ni kukusanya bilioni 318.

Nzige hao wamevamia nchi sita za Afrika Mashariki na wana uwezo wa kula chakula sawa na watakachokula watu 35,000 kwa siku moja wakiwa kwenye eneo la kilomita 1 ya mraba, FAO imeeleza.

Nzige hao wanazaliana kwa kasi kubwa sana katika mazingira rafiki ambapo ndani ya kipindi cha miezi sita wanauwezo wa kuongezeka kwa zaidi ya mara 500.