Rais FĂ©lix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo – DRC, ametangaza Baraza la Mawaziri la nchi hiyo ikiwa imepita miezi Saba tangu aapishwe kuliongoza Taifa hilo.
Mwezi Disemba mwaka 2018, Rais Tshisekedi ambaye ni mtoto wa Mwanasiasa wa muda mrefu wa upinzani wa DRC Hayati Etienne Tshisekedi, alishinda uchaguzi wa kwanza wa Kidemokrasia tangu Taifa hilo lipate uhuru wake kutoka Ubelgiji mwaka 1960.
Mwezi Julai mwaka huu Rais Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila, walikubaliana kuunda serikali ya Umoja itakayokua na Mawaziri 66.
Kama ilivyo katika makubaliano hayo, Chama cha Kabila cha PPRD kimepata wizara 43 na kile cha Rais Tshisekedi kimepata wizara 23 katika serikali hiyo ya Umoja.
Habari zaidi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zinasema kuwa, kuna sura mpya katika Baraza hilo jipya la Mawaziri ambazo hazijawahi kuwepo katika serikali na pia imeundwa Wizara maalum kwa ajili ya kushughulikia watu wenye Ulemavu.
Katika Baraza hilo la Mawaziri, Wanawake wamepewa asilimia 17 na Wanaume asilimia 83.