Balozi za Afrika Kusini nchini Nigeria zafungwa kwa muda

0
308

Afrika Kusini imefunga kwa muda Balozi zake zilizopo nchini Nigeria, kufuatia mashambulio ya kulipiza kisasi yanayofanywa na raia wa nchi hiyo kwa kile wanachodai kuwa raia wa Nigeria wamekua wakishambuliwa Afrika Kusini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, – Naledi Pandor amesema kuwa tayari ameagiza kufungwa kwa ofisi hizo za Ubalozi ziliopo katika Mji Mkuu wa Nigeria, – Abuja na zilizopo Lagos, kufuatia vitisho vinavyotolewa dhidi ya Wafanyakazi wa Balozi hizo.

Pandor amesema kuwa, serikali ya Afrika Kusini imesikitishwa na vurugu

zinazoendelea nchini humo za kuwashambulia wageni zinazofanywa na baadhi ya raia wa nchi hiyo na kuziomba nchi nyingine kutolipiza kisasi kwa raia wake waliopo katika nchi hizo.

Kwa siku kadhaa sasa, makundi ya raia wa Afrika Kusini yamekua wakivamia maduka na kuiba pamoja na kuharibu bidhaa, na kuwashambulia wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Maandamano yamefanyika katika maeneo mbalimbali nchini Nigeria, ambapo raia wa nchi hiyo wameharibu mali za Wafanyabiashara wa Afrika Kusini waliopo nchini humo huku ikielezwa kuwa kampuni kubwa ya simu ya MTN ya nchini Afrika Kusini imefunga ofisi zake nchini Nigeria kwa hofu ya kushambuliwa.

Tayari Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ametuma maafisa wake nchini Afrika Kusini ili kuangalia hali ya raia wake waliopo nchini Afrika Kusini.