AU yaionya Sudan

0
298

Baraza la Amani na Ulinzi la Umoja wa Afrika limeipa Serikali ya Mpito ya Kijeshi ya Sudan muda wa siku 15 uwe umekabidhi madaraka kwa utawala wa Kiraia, la sivyo nchi hiyo itasimamishwa uanachama wa Umoja wa Afrika.

Katika taarifa yake iliyotolewa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, Baraza hilo limesema kuwa kuwepo kwa Serikali hiyo ya Mpito ya Kijeshi  ya Sudan kutazusha machafuko,  kwa kuwa hayakua matarajio ya raia wa nchi hiyo.

Wakati hayo yakiendelea, waandamanaji wanaoipinga serikali ya Mpito ya Kijeshi nchini Sudan bado wako nje ya Makao Makuu ya jeshi la nchi hiyo, wakishinikiza serikali hiyo kurejesha utawala wa Kiraia.

Wamedai kuwa Jeshi la Sudan limeteka maana ya maandamano yao, kwani walimtoa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Al Bashir madarakani ili kupata utawala mpya wa kiraia na sio utawala wa kijeshi unaowakandamiza.