APC yawashukuru Wananchi kwa ushindi

Uchaguzi Nigeria

0
210

Chama tawala cha nchini Nigeria cha All Progressives Congress (APC) kimewashukuru wananchi wa Taifa hilo kwa kumpa kura nyingi mgombea wake Bola Tinubu,
na hivyo kumuwezesha kuwa Rais mpya wa nchi hiyo.

Tume ya Uchaguzi ya Nigeria imemtangaza Tinubu kuwa mshindi wa kiti hicho cha Urais kufuatia uchaguzi uliofanyika Jumamosi iliyopita nchini humo na kuwashinda wagombea wengine 17.

Tinubu mwenye umri wa miaka 70, Mwanasiasa mkongwe na Gavana wa zamani wa Lagos, ametangazwa mshindi baada ya kupata kura
8,794,726 ambazo ni sawa na asilimia 36 na kuwabwaga wapinzani wake wawili wa karibu.

Wapinzani hao ni Atiku Abubakar ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais wa Nigeria na aliyewania kiti hicho kwa mara ya sita.

Mwingine ni Peter Obi, Gavana wa zamani wa jimbo la Anambra, aliyekuwa mgombea kutoka chama cha Leba.

Wagombea hao wawili wametangaza kuyakataa matokeo hayo ya Urais na kutaka uchaguzi huo ufutwe na ufanyike upya wakiituhumu Tume ya Uchaguzi ya Nigeria kwa kushindwa kushughulikia changamoto kadhaa zilizojitokeza.

Mshindi wa kiti cha Urais nchini Nigeria alitakiwa kupata asilimia 25 ya kura zote zilizopigwa katika majimbo 24 kati ya 36 ya nchi hiyo na endapo kusingekuwa na na mshindi, kungekuwa na duru ya pili ya uchaguzi baada ya siku 21 kati ya mshindi wa kwanza na wa pili.