Majaji nchini Marekani wamemkuta na hatia afisa wa polisi wa zamani wa nchi hiyo, kufuatia kifo cha raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika, George Floyd.
Mwezi Mei mwaka 2020 huko Minneapolis, Derek Chauvin mwenye umri wa miaka 45 alinaswa katika mkanda wa video akipiga goti kwenye shingo ya Floyd kwa zaidi ya dakika tisa.
Mkanda huo wa video ulitazamwa na watu wengi na kuibua hisia kali, hali iliyosababisha maandamano yaliyokuwa na lengo la kupinga ubaguzi wa rangi na polisi kutumia nguvu kupita kiasi wanapokabiliana na raia.
Chauvin ataendelea kuwa kizuizini hadi atakapohukumiwa na huenda akakabiliwa na kifungo cha miongo kadhaa jela.
Wakili wa familia ya Floyd, – Ben Crump amepongeza uamuzi huo uliotolewa na majaji hao wa Marekani na kusema kuwa ni wa historia ndani ya Taifa hilo.
Rais Joe Biden wa Marekani na Makamu wake Kamala Harris wameipigia simu familia ya Floyd mara baada ya uamuzi huo.