Algeria yajiandaa kuunda serikali

0
297

Waziri Mkuu wa Algeria, – Roureddone Bedoui amesema kuwa serikali yake inaandaa mchakato wa uundaji wa serikali mpya, serikali itakayowajumuisha watu wa kada mbalimbali na umri tofauti ili kukidhi mahitaji ya raia wa nchi hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Algiers, -Bedoui amesema kuwa serikali mpya itajumuisha vijana na wanawake, ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawashirikishwi katika muundo wa serikali.


Mwanasiasa huyo amesema kuwa serikali mpya wa Algeria atakayoiunda pia itawajumuisha watu walioshiriki katika vuguvugu la maandamano ya kupinga serikali ya nchi hiyo, kwani lengo la maandamano hayo lilikuwa ni kutaka mabadiliko.


Waziri Mkuu wa Algeria amelazimika kuitisha mkutano na waandishi wa habari, baada ya mfululizo wa maandamano ya wananchi kupinga serikali ya Rais Abdelaziz Bouteflika wa nchi hiyo, hasa alipoazimia kugombea tena Urais.


Wananchi wa Algeria wengi wao wakiwa ni vijana hasa wanafunzi wa vyuo vikuu, wamekuwa wakiandamana nchini Algeria kupinga hatua ya Bouteflika anayetibiwa nje ya nchi kugombea urais kwa muhula wa Tano.


Bedoui ameongeza kuwa Rais Bouteflika ametangaza kuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo umeahirishwa kwa maslahi ya wananchi wa Taifa hilo ili kufanyia marekebisho sheria kadhaa kwa kupitia Tume maalum iliyoteuliwa na Rais.


Amewataka viongozi wa vyama vya upinzani nchini humo kukubali mabadiliko na kushiriki katika mchakato wa kufanya marekebisho ya nchi hiyo yakiwemo ya katiba.