Rais Omar Al Bashir wa Sudan amekuwa kiongozi wa kwanza kutoka Umoja wa nchi za Kiarabu kuitembelea Syria, tangu nchi hiyo iingie kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe takribani miaka nane iliyopita.
Katika uwanja wa ndege wa Damascus , -Al-Bashir amepokelewa na mwenyeji wake Rais Bashar Al Assad wa Syria kabla ya viongozi hao kuelekea Ikulu ambapo wamefanya mazungumzo juu ya uhusiano wa nchi hizo mbili na maendeleo ya Syria pamoja na ya Mashariki ya Kati.
Syria ilifukuzwa uanachama wa mataifa 22 ya Umoja wa nchi za Kiarabu baada ya kuingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011.
Nchi za Kiarabu zimeiwekea Syria vikwazo na mara kwa mara zimekuwa zikimlaumu Rais Al Assad kwa kutumia nguvu kubwa ya kijeshi na pia kushindwa kwake kujadiliana na wapinzani.
Lengo la ziara ya Rais huyo wa Sudan, -Omar Al Bashir nchini Syria halijawekwa wazi, lakini kutokana na kuwa vita inaendelea kupungua nchini humo na vikosi vya serikali vikiendelea kuikomboa miji kadhaa muhimu, baadhi ya viongozi wa mataifa ya Kiarabu wameonyesha nia ya kutaka kurejesha uhusiano na serikali ya Syria.