Ajali yaua hamsini Kenya

0
1897

Watu hamsini wamekufa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutumbukia bondeni kwenye barabara kuu ya Nairobi – Kisumu nchini Kenya.

Vyombo vya habari nchini Kenya vimesema kuwa ajali hiyo mbaya imetokea katika eneo la Fort Ternan lililopo kwenye jimbo la Kericho majira ya alfajiri.

Kamanda wa polisi wa jimbo la Kericho, – James Mogera amesema kuwa dereva wa basi hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 67 alishindwa kulimudu na kisha kuvigonga vizuizi vilivyokuwa kando ya barabara na mwisho kutumbukia bondeni.

Awali jeshi la polisi nchini Kenya lilisema kuwa idadi ya watu waliokufa ni arobaini, lakini baadae likasema kuwa idadi hiyo imeongezeka kutokana na majeruhi waliokua na hali mbaya kufariki dunia.

Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo wanatibiwa katika zahanati ya Fort Ternan na wengine kwenye hospitali ya jimbo la Muhoroni.

Taarifa zaidi  kutoka nchini Kenya zinasema kuwa miili ya baadhi ya watu waliokufa katika ajali hiyo imeshindwa kunasuliwa kutoka ndani ya basi hilo.