Airbus kutotengeneza A380

0
1116

Kampuni ya kutengeneza ndege ya Airbus yenye  Makao Makuu yake nchini Uholanzi  imetangaza kusimamisha utengenezaji wa ndege kubwa aina ya A380 “Superjumbo” katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Tangazo hilo la Airbus linafuatia kampuni ya ndege ya Emirates ambayo ni mteja mkubwa wa ndege hizo kupunguza uhitaji kutoka ndege 162 hadi kufikia 123.

Badala yake  Airbus imesema kuwa itajielekeza katika utengenezaji wa ndege za saizi ya kati

Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo ya Airbus imesema kuwa ndege ya mwisho ya A380  itatengenezwa  mwaka 2021  na baada ya hapo hazitatengenezwa tena, na hivyo kuifanya ndege hiyo ya mwisho kuwa miongoni mwa ndege ambazo utengenezaji wake umekuwa wa muda mfupi sana.

Airbus walianza kutengeneza ndege hiyo  aina ya A380 ili kutoa ushindani kwa ndege za Boeing 747 Jumbo Jet, lakini hata hivyo Boeing haikuingia katika ushindani huo na  badala yale ilitengeneza ndege aina ya Boeing Dreamliner na Boeing 787 kwa madai kuwa wataendelea kutengeneza ndege za saizi ya kati na kuiboresha ndege aina ya Boeing 747.

Wachunguzi mbalimbali wa masuala ya kiuchumi duniani wamesema kuwa ili kukidhi mahitaji ya Airbus A380,  nchi nyingi ziliingia gharama  ya kurekebisha viwanja vyao ili ndege hiyo iweze kutua na kuhudumiwa na hivyo kufuatia hatua ya Airbus kutotengeneza tena ndege hiyo ina maana nchi hizo ziliingia gharama zisizo na msingi katika kurekebisha viwanja hivyo.

Kwa mujibu wa wachunguzi hao, wanunuzi wa A380 si wengi kama Airbus ilivyotarajia na kwamba Boeing walikuwa sahihi kusita kuingia katika ushindani wa kutengeneza ndege kubwa za aina hiyo.

Mamia ya wafanyakazi wanatarajiwa kupoteza ajira kutokana na hatua ya kampuni hiyo ya Airbus kusimamisha uzalishaji huo wa ndege zake aina ya A380 “superjumbo”.