Wawekezaji wazawa watakiwa kushirikina na wale wa nje

0
2007

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji  Angellah Kairuki amewataka wawekezaji wazawa kushirikina na wawekezaji kutoka nje ili kupata ujuzi, maarifa na kukuza mitaji na hivyo kupanua sekta ya uwekezaji nchini.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa uwekezaji na wawekezaji kutoka nchini China, Waziri Kairuki amesema kuwa wawekezaji  wazawa wanapaswa  kushirikiana na wawekezaji kutoka nje kwa kuingia ubia na kampuni za huko ili kuchukua ujuzi katika sekta mbalimbali walizowekeza nchini.

Mkutano huo umeshirikisha wawakilishi wa kampuni 200 kutoka nchini china, taasisi 25 za Umma na Maafisa waandamizi wa Serikali za China na Tanzania, lengo likiwa ni kujadili na kuangalia changamoto kwa wawekezaji wa kutoka nchini humo ili ziweze kutatuliwa haraka.

Waziri Kairuki ameishukuru serikali ya China kupitia ubalozi wake hapa nchini kwa kuweza kufanikisha mkutano huo uliowakutanisha wawekezaji wa nchi hiyo ambao wamewekeza Tanzania kwenye miradi mingi inayowasaidia wananchi na nchi kwa ujumla.

“Wawekezaji kutoka China wamewekeza mtaji wa Dola Bilioni Saba za Kimarekani, si kiasi kidogo,  naamini wametoa mchango mkubwa kwenye ajira, maendeleo yetu, na sekta zingine za kiuchumi hapa nchini, kwa hiyo uwekezaji huu wa miradi mingi ni fursa kwa wananchi wetu, tutaendelea kuweka mkazo kuhakikisha kuwa changamoto zinaondolewa”, amesema Waziri Kairuki.