Wailer wa The Wailers afariki dunia

0
320

Nyota wa muziki wa reggae kutoka nchini Jamaica, – Bunny Wailer ambaye alishirikiana na Bob Marley kuunda kundi la The Wailers mwaka 1963 amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 73.

Wizara ya Utamaduni ya Jamaica imesema kuwa Wailer ambaye jina lake halisi ni Neville Livingstone alipata kiharusi mwaka 2018 na tangu mwezi Desemba mwaka 2020 alikuwa amelazwa katika hospitali moja jijini Kingston.

Wailer alikuwa ndiye mwanamuziki aliyesalia hai kwa waanzilishi wa kundi hilo la The Wailers, mwingine ni Bob Marley aliyefariki dunia  mwaka 1981 baada ya kuugua saratani na Peter Tosh aliuawa mwaka 1987.

Wailer ambaye alikuwa rafiki wa Marley toka utotoni, katika uhai wake amewahi kushinda tuzo tatu za Grammys na mwaka 2017 alitunukiwa tuzo ya heshima nchini Jamaica (Order of Merit) ambayo ni moja ya heshima kubwa nchini humo.

Nyimbo maarufu za kundi hilo la The Wailers ni pamoja na Simmer Down na One Love.