Mwanamuziki wa miondoko ya kufoka, Mwandishi wa nyimbo, Mwigizaji na Mshairi kutoka nchini Afrika Kusini, -Maya Christinah Xichavo Wegerif anayejulikana kisanii kwa jina la Sho Madjozi, amepatwa na mshangao mkubwa nusura kupoteza uhai baada ya kukutana ana kwa ana na nyota wa mieleka kutoka nchini Marekani, – John Cena.
Sho Madjozi amekutana na Cena katika kipindi kinachotangazwa mara moja kwa wiki na mwimbaji Kelly Clarkson kinachojulikana kama The Kelly Clarkson Show ambacho ni cha saa moja, huku kikibeba hadithi za kusisimua, maonesho ya muziki ya moja kwa moja na michezo.
Madjozi mwenye umri wa miaka 27 alikaa na Clarkson kwa mahojiano yaliohusu mambo kadhaa kabla ya kumpatia nafasi ya kutoa burudani ya kuimba wimbo wake maarufu uitwao John Cena, ambao unavuma sana kutokana na ufundi uliowekwa katika mistari, midundo na uchezaji.
Wimbo huo una mchanganyiko wa lugha mbalimbali, ikiwemo ile ya Kiswahili.
Alipoulizwa kama angepata nafasi ya kukutana na John Cena ingekuaje, Sho Madjozi akajibu kuwa, ana matumaini ya kukutana na nyota huyo wa Mieleka siku moja, na ikitokea hivyo basi itakua furaha kubwa kwake.
“John alishwahi kupost wimbo wangu katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, ila hajawahi kusema chochote, nampenda sana John Cena na ikiwa nitaonana naye nitawehuka”, alisema Madjozi.
Mtangazaji Kelly katika mahojiano hayo alimdanganya Sho Madjozi kwa kusema kwamba John Cena hayupo kwenye kipindi cha siku hiyo kutokana na bajeti kuwa ndogo, lakini kumbe mambo yalikua tofauti.
Sho Madjozi alianza kuimba pasipo kujua John Cena yupo na anamsogelea, baada ya sekunde chache akashtuka baada ya kumuona, ndipo alipochanganyikiwa na kuacha kuimba huku akipiga kelele kwa furaha na baadaye kwenda kumkumbatia kwa furaha.
Sho Madjozi ambaye ni mmoja wa Wasanii bora nchini Afrika Kusini, amekua akidumisha utamaduni wa Kiafrika kwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mavazi yake na lugha kupitia muziki wake.
Madjozi amewahi kusafiri na baba yake hadi katika jiji la Dar es salaam nchini Tanzania, ambako ndiko alijifunza lugha ya Kiswahili.
Miongoni mwa maneno ya Kiswahili katika wimbo wake huo wa John Cena ni pale anaposema “Unajifanya hunioni labda mimi John Cena ulinifanya mfungwa wako labda mi ni Madiba
Sina plan, sina cash, hata pesa mi sina Eeh ndo maana unanitreati kama nimekuibia Lakini mimi nimekupenda though I don’t know why you treat me like a criminal, eish”.