Sasa nimebadilika: Chid Benz

0
1699

Naibu Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza amesema wizara hiyo itaendelea kushirikiana na msanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva) Rashid Abdallah maarufu kama Chid Benz pamoja na wasanii wengine.

Naibu Waziri Shonza ametoa ahadi hiyo jijini Dodoma alipokutana na Chid Benz, ambaye amemuhakikishia kuwa kwa sasa amebadilika na anataka kuwaonesha Watanzania kuwa ameachana na matumizi ya dawa za kulevya.

“Kati ya wasanii wenye kukubalika na mashabiki zao, wewe Chid Benz ni mmoja wao na mashabiki zako ni wengi, hivyo ningependa kukuona kuanzia sasa unalijenga zaidi  jina lako kwa kuonesha kuwa umebadilika, katika kipindi hiki nitafurahi zaidi kukuona unasonga mbele na hurudi tena katika matumizi ya dawa za kulevya. Wizara ipo pamoja na wewe kukusaidia wakati wowote,” amesema Naibu Waziri Shonza.

Naye Chid Benz amesema kwa sasa hatajihusisha tena na mambo ambayo ni kinyume na maadili ya Mtanzania na kwamba anachohitaji ni kuwapa kile ambacho mashabiki wake wanakihitaji.

 “Ombi langu kwa serikali ni kupata ushirikiano, na mapema wiki ijayo ninatarajia kutoa wimbo wangu mmoja uitwao “Beautiful” ambao nimeuiamba nikisifu uzuri wa mwanamke,  na kufuatia janga la corona ninamuahidi mheshimiwa naibu waziri kuwa nitatunga wimbo kwa ajili ya corona,” amesema Chid Benz.