Mrembo Queen Elizabeth Makune ambaye ni Mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo cha Uhasibu kutoka jijini Dar es salaam amevikwa Taji la Miss Tanzania baada ya kuwabwaga warembo wengine katika shindano lililofanyika Septemba Nane mwaka huu.
Kufuatia ushindi huo, Queen Elizabeth ataungana na warembo wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani kushiriki shindano kubwa la urembo la Dunia yaani Miss World litakalofanyika huko Sanya nchini China Disemba Nane mwaka huu.
Warembo walioingia Tano bora katika kinyang’anyiro hicho ni Queen Elizabeth Makune kutoka Dar es salaam, Nelly Kalikanzi kutoka Dar es salaam, Linda Samson kutoka Dar es salaam, Sandra Loren kutoka Kanda ya Kaskazini na Sharon Headlam kutoka Kanda ya Ziwa.
Washiriki wa shindano hilo ambalo mgeni rasmi alikua Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe walionesha aina mbalimbali ya mavazi likiwemo lile la kanga na la ubunifu.
Kinyang’anyiro hicho kilishirikisha walimbwende Ishirini kutoka maeneo mbalimbali nchini.