Rapa Kanye Omari West maarufu kama Kanye West kutoka nchini Marekani, ameendelea kumtumikia Mungu katika kanisa la Lakewood Mega huko Houston, linaloongozwa na Mtumishi Joel Osteen wa nchini humo.
Kanye ambaye mwenyewe anajiita msanii mkubwa na bora kuwahi kuishi duniani, Jumapili iliyopita aliongoza ibada katika kanisa hilo huku akiimba nyimbo za dini ya Kikristo ambazo baadhi zipo katika albamu yake ya muziki ya mwaka huu.
Katika ibada hiyo, Rapa huyo ambaye pia mwandishi na mtayarishaji wa nyimbo, mjasiriamali na mbunifu wa mavazi, alitoa mahubiri yenye maneno yanagusa maisha yake ya kiroho hasa wito alionao kwa Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwa picha za video zilizosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kutoka kanisani hapo zinamuonyesha Kanye West akicheka kwa furaha.
“Ninajua kuwa Mungu amekuwa akiniita kwa muda mrefu na Ibilisi naye amekuwa akinipotosha kwa muda mrefu, nilipokuwa chini kabisa Mungu alikuwa pamoja nami na kunitia moyo”, amesema Kanye.
Kanye Omari West mwenye umri wa miaka 42 ni mume wa Mwanamitindo Kim Kardashian, ambao wamejaliwa kupata watoto Wanne ambao ni Saint West, Psalm West, North West na Chicago West.
Kwa muda mrefu Kanye amekua na mpango wa kuanzisha kanisa lake la huduma ya kila Jumapili na katika siku za hivi karibuni imeelezwa kuwa amekua akitoa huduma hiyo nyumbani kwake na pia katika mitaa mbalimbali.