Familia za Mzee Majuto na Steven Kanumba zalipwa milioni 85.

0
435

Serikali imesema kuwa imeokoa na kurejesha mamilioni ya fedha kwa familia za marehemu Mzee Majuto pamoja na familia ya marehemu Steven Kanumba kupitia mikataba ya kazi walioingia wakiwa hai.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi katika hafla ya kukabidhi nyaraka za uhamishaji wa COSOTA kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kwenda Wizara ya Habari.

“Familia ya Marehemu Mzee Majuto mpaka sasa tumewarejeshea TZS milioni 65 na familia ya Marehemu Steven Kanumba tumeirejeshea TZS milioni 20 kutoka katika mikataba ya kazi waliyokuwa wameingia,” amesema Dkt. Abbasi .

Aidha, amewahakikishia wasanii kuwa serikali ipo macho na inalinda kazi zao kuhakikisha wananufaika na sanaa na sio kuwa masikini wenye majina maarufu.

Zoezi la kuhamisha COSOTA limekamilika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Julai 12 mwaka huu jijini Dodoma akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, wasanii na wageni wengine aliowaalika Ikulu ya Chamwino kwa ajili ya chakula cha mchana.