BASATA yawafungia Diamond na Rayvan

0
1250

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA ) limewafungia kwa muda usiojulikana wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Nassib Abdul maarufu kama Diamond na Raymond Mwakyusa maarufu kama Rayvan kufanya onesho lolote ndani na nje ya nchi.

Taarifa iliyotolewa na BASATA imesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na wasanii hao kukiuka maagizo ya Baraza hilo kwa kuimba wimbo wa Mwanza uliofungiwa kutokana na kukiuka maadili.

BASATA pia imesitisha kibali cha tamasha la Wasafi Festival kwa mwaka 2018, tamasha lililokua likifanywa na wasanii hao kutokana ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu katika uendeshaji wake.

Novemba 12 mwaka huu, BASATA ilitoa taarifa kwa umma ya kuufungia wimbo unaojulikana kwa jina la Mwanza ulioimbwa na Diamond pamoja na Rayvan na kupiga marufuku kutumbuizwa sehemu yoyote.

Hata hivyo wasanii hao wameshindwa kutii agizo hilo na kuendelea kuuimba wimbo huo katika matamasha yao mbalimbali.