Diamond afikishwa mahakamani kwa uharibifu wa mali

0
1747

Kesi ya uharibifu wa mali inayomkabili mwanamuziki Naseeb Abdul maarufu kwa jina la Diamond Platnumz imeahirishwa hadi Machi 18 mwaka huu.

Katika kesi ya msingi Diamond amefikishwa katika Mahakama ya Ardhi Mwananyamala jijini Dar es salaam, akishtakiwa kwa tuhuma za uharibifu wa mali zenye thamani ya shilingi milioni 337.

Diamond ambaye amekuwa akifanya vizuri kwenye muziki ndani na nje ya nchi, anatuhumiwa kutenda kosa hilo katika nyumba aliyokuwa amepanga kwa matumizi ya studio eneo la Sinza.

Mmiliki wa nyumba hiyo, Maulid Wandwe amesema fedha hizo zinajumuisha kodi ya nyumba ya mwaka mmoja, ambayo mwanamuziki huyo anadaiwa.

Wakili wa Diamond, Gerald Hamisi amesema mteja wake yupo nje ya nchi, na hatorejea nchini katika siku za karibuni kutokana na mlipuko wa homa ya mapafu, COVID-19, inayosababishwa na virusi vya corona.