Davido: Sina mpango wa kuwa mwanasiasa

0
2886

Mwanamuziki Davido kutoka nchini Nigeria amesema kuwa hana mpango wa kuingia kwenye siasa kwa sababu kufanya hivyo kutafuta yote mazuri na makubwa aliyofanya kwenye tasnia ya burudani.

Davido ambaye jina lake ni David Adeleke amesema mbali na muziki anapenda habari na siasa, lakini hana mpango wa kuwa mwanasiasa kwani siasa nchini mwao ni vurugu.

“Siwezi kuharibu miaka yangu yote ya kuburudisha, kuwafanya watu kuwa na furaha, nibadili na kuwa mwanasiasa na yote niliyofanya kama Davido, na kila kizuri nilichojifanyia vipotee, kwani najua hicho ndicho kitakachotokea,” amesema Davido.

Amesema kwa namna familia yake ilivyo, njia alivyoichukua ni tofauti kabisa kwani alitarajiwa asome, na atakapohitimu akamsaidie baba yake, ambaye ni mfanyabiashara, kwenye kazi zake.

Ameeleza zaidi kwamba awali baba yake alikuwa na mashaka na uchaguzi wake, lakini hofu yake iliisha alipoachiwa wimbo wake wa Dami Duro mwaka 2012, ambao ulimtambulisha kwenye muziki.

Nigeria kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa mafuta ya magari, migomo wa wanafunzi wa chuo kikuu na hofu kuhusu hali ya usalama.