Cardi B kutumbuiza kwenye tamasha kubwa la Livespot X

0
1529

Mwanamuzi wa Kike wa miondoko ya Rap kutoka nchini Marekani, – Belcalis Marlenis maarufu kama Cardi B yupo nchini Nigeria, kwa ajili ya kutumbuiza katika tamasha kubwa la muziki linalojulikana kama Livespot X litakalofanyika hapo kesho.

Cardi B mwenye umri wa miaka 27, ametumia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Instagram kuwaeleza mashabiki wake kuwa yupo nchini Nigeria,  na kueleza furaha yake kwa kufika nchini humo ikiwa ni mara yake ya kwanza.

Katika mtandao huo wa kijamii wa Instagram, Rapa huyo ambaye pia ni mshindi wa Tuzo za  Grammy kwa mziki wa Rap, ameweka picha ya Video ikimuonyesha akicheza wimbo wa Fall Remix ambao ameshirikishwa na Mwanamuziki nyota wa Nigeria, – Davido.

Tayari video hiyo imefikisha Watazamaji zaidi ya Milioni Sita na maoni zaidi ya Elfu 18.

Fall ni wimbo uliomtambulisha vyema Davido katika soko la muziki Duniani na sasa upepo wake umezidi kuwa mkali zaidi baada ya Cardi B kutangaza ujio huo wa Remix ya ngoma hiyo kali, ambayo hata hivyo bado haijatoka.

Wimbo huo utakuwa ni wa kwanza kutoka kwa Rapa huyo wa kike anayesumbua zaidi game la muziki wa Hip Hop nchini Marekani kwa sasa, na Mwanamuziki mkubwa kutoka Afrika.

Akiwa nchini Nigeria Cardi B atatumbuiza katika tamasha hilo la Livespot X litakalofanyika katika mji wa Lagos hapo kesho Jumamosi, kabla ya kuelekea nchini Ghana ambapo siku ya Jumapili atatumbuiza kwenye tamasha jingine la muziki la Livespot X, ambalo litafanyika katika uwanja wa michezo uliopo kwenye mji mkuu wa  nchi hiyo, –  Accra.