Wawekezaji katika sekta ya ngozi wamewasili hapa nchini wakitokea Misri, kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipofanya ziara nchini humo mwezi Julai mwaka huu na kukutana na wawekezaji hao.
Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt Felix Nandonde amesema kuwa wakati wa ziara yake nchini Misri, Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea mji wa viwanda vya ngozi wa Roubiki na kuzungumza na Wawekezaji hao, ambapo aliwataka kufanya ziara nchini na kuangalia namna ya kuwekeza katika sekta ya ngozi kutokana na ubora wa bidhaa ya ngozi inayopatikana Tanzania.
Dkt Nandonde amesisitiza kuwa, Serikali ina imani kuwa wawekezaji hao watapanga mipango ya muda mrefu na mfupi kuhakikisha sekta ya ngozi Tanzania inakua na manufaa kwa Wafugaji na Taifa.
Mara baada ya kuwasili nchini, Wawekezaji hao katika sekta ya ngozi kutoka nchini Misri walitembelea kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Woiso kilichopo Salasala jijini Dar es salaam wakiwa na lengo la kujionea namna ngozi inavyotumika kutengenezea bidhaa mbalimbali.
Wakiwa kiwandani hapo, Wawekezaji hao wameshuhudia idadi kubwa ya vijana walioajiriwa wakiwa katika majukumu yao ya kutengeneza bidhaa mbalimbali vikiwemo viatu, mikanda na mabegi.