Wenye maeneo ya uwekezaji watakiwa kushirikiana na TIC

0
2242

Watanzania wenye viwanja na maeneo makubwa nchini ambayo yanafaa kwa uwekezaji wameshauriwa kwenda katika Kituo cha Uwekezaji nchini – TIC ili kuona ni kwa namna gani wataweza kuyatumia maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wawekezaji kutoka TIC, –  Ayoub Sizya wakati alipotembelea na kukagua eneo la ukanda wa uwekezaji na mauzo ya ndani na nje ya nchi la Kilua lililopo  katika kijiji cha Disunyala kata ya Mlandizi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

TIC imeingia makubaliano na mmiliki wa  eneo hilo lenye zaidi ya ekari elfu moja ambalo ni maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.

“Sisi TIC tumeingia makubaliano na Ukanda huu wa uwekezaji wa Kilua,  lengo letu ni kuimarisha shughuli za uwekezaji,tunafanya hivi ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi,kama unavyojua eneo hili linamilikiwa na mtu binafsi,na ni eneo kubwa ,hivyo tukiungana tutaleta wawekezaji wengi zaidi na Tanzania ya viwanda itazidi kusonga mbele”, amesema  Sizya.

Kwa upande wake mmiliki wa eneo hilo la ukanda wa uwekezaji Mohammed Kilua amesema kuwa wanatarajia kujenga zaidi ya viwanda sabini  na kwamba mpaka sasa kiwanda kimoja kimekamilika ujenzi wake huku vingine saba vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

“Tutajenga viwanda vingi, ni zaidi ya 70 na kwenye eneo hili tayari tumepata maombi ya zaidi ya ujenzi wa viwanda 20 kwa mwaka huu, Tanzania ya Viwanda itafanikiwa tu,lengo letu ni kuunga mkono juhudi za Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli” ameongeza Kilua.

Kampuni ya Kamaka ambayo ni moja ya kampuni zilizowekeza  katika eneo hilo la Kilua imesema kuwa ushirikiano baina ya Kilua na TIC utaleta tija ya uzalishaji wa viwanda na kufikia lengo la serikali la kuwa na uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati.

Mpaka sasa, eneo hilo la ukanda wa uwekezaji na mauzo ya ndani na nje ya nchi la Kilua lililopo katika kijiji cha Disunyala kata ya Mlandizi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani limetumia zaidi ya shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kuweka miundombinu ya umeme,maji na barabara.