Wafanyabiashara wa Russia waonyesha nia ya kuwekeza Tanzania

0
3444

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza Ubalozi wa Tanzania nchini Russia kuratibu mipango ya Wafanyabiashara wa nchi hiyo wanaokusudia kuwekeza nchini kwa kuwaunganisha na Taasisi na Wizara husika.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya kugundua uwepo wa Wafanyabiashara wengi wa Russia wanaokusudia kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji pamoja na kutafuta Wafanyabiashara wa Kitanzania watakaoungana nao katika uwekezaji wanaokusudia kuufanya.

 “Tayari miadi imekwishawekwa ya kuwakaribisha Wawekezaji wa Russia kuja Tanzania kwa ushawishi wa kwangu mwenyewe pamoja na ushawishi wa Wafanyabiashara wa Tanzania, hivyo nisingependa Wafanyabiashara hao wasumbuliwe au kukatishwa tamaa katika kutimiza nia yao hiyo”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Ameongeza kuwa, mkutano baina ya Wakuu wa nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Russia  uliomalizika katika mji wa Sochi, ulilenga kujenga uhusiano mzuri zaidi katika nyanja mbalimbali hususani za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Russia imeutumia mkutano huo kueleza bayana maeneo ambayo wako tayari kushirikiana na Afrika katika kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na uuzaji wa zana za kilimo, uwekezaji katika sekta za mafuta, gesi na madini na ujenzi wa miundombinu hasa reli.

Leo Waziri Mkuu Majaliwa anaondoka nchini Russia na kuelekea nchini Azerbaijan ambako pia atamwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano wa siku Mbili wa nchi zisizofungamana na upande wowote.