Ufugaji wa samaki kuongeza malighafi viwandani

0
4678

Serikali imesema uwekezaji wa ufugaji wa samaki utasaidia kuongeza malighafi kwenye viwanda vya uchakataji wa samaki pamoja na kuanzisha viwanda vipya hususani katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema hayo wakati alipotembelea shamba la ufugaji samaki linalomilikiwa na Kampuni ya Tanlapia lililopo wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya kuona shughuli zao za ufugaji wa samaki na namna wadau ambao serikali inataka wafanikiwe katika ufugaji wa samaki ili kufikia lengo la kuzalisha samaki kwa wingi ifikapo mwaka 2025 na kufikia kiwango sawa cha samaki wanaovunwa kupitia maji ya asili.

“Kwa sasa tuna viwanda vingi kidogo na vingine vinazalisha chini ya viwango kutokana na kukosa malighafi, sasa uzalishaji kama huu utasaidia viwanda kuwa na malighafi hususani katika ukanda wa bahari ambao una viwanda vichache vya kuchakata mazao ya samaki na bado tunataka uzalishaji huu uendelee ili kuzalisha viwanda ambavyo tayari vimesimikwa katika ukanda wa bahari na kusafirisha bidhaa za samaki nje ya nchi,” amesema Ndaki

Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuhakikisha inaendeleza wawekezaji hapa nchini ili kufikia malengo ya uzalishaji mkubwa wa samaki kupitia ufugaji wa samaki.

Aidha, amesema mwelekeo wa serikali ni kuwatia moyo wazalishaji wakubwa wa samaki ili uwekezaji uwe na tija kwa taifa kwa kupatikana kwa chakula na ajira kwa nchi.

Amesema kupitia shamba la Tanlapia ambalo katika awamu ya kwanza linatarajia kuwa na mabwawa 48 ya samaki, kuwa shamba darasa la watu kutoka maeneo mbalimbali nchini kujifunza namna ya ufugaji wa samaki kibiashara.