Tumekamilisha malipo yote ya Korosho : Waziri Mkuu

0
3478

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, malipo yote ya korosho kwa msimu uliopita yamekamilika, na sasa serikali inamalizia malipo ya Tani Elfu 25 pekee zilizobaki huku kazi ya kuzisomba korosho hizo kutoka katika maghala mkoani Lindi na Mtwara ikiendelea.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa, Bodi ya Mazao Mchanganyiko imepewa jukumu la kumalizia malipo ya wamiliki wa maghala ya kuhifadhi korosho na madeni mengine yaliyotokana na zoezi hilo.

Akisoma hotuba ya kuahirisha mkutano wa 16 wa Bunge jijini Dodoma Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, tayari serikali imekwishanunua Tani 199 kati ya Tani 222.8 za korosho zote zilizovunwa msimu wa mwaka 2018.

Aidha katika kusimamia ununuzi wa korosho kwa msimu wa mwaka huu, Serikali imeweka mazingira ya kuwezesha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya korosho ili viweze kununua korosho kutoka kwa Wakulima na kuziongezea thamani.

Hata hivyo Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, kupitia wizara ya Kilimo, Serikali inaendelea kuratibu soko la zao la korosho ili kasoro zilizojitokeza katika msimu uliopita zisijitokeze tena msimu huu.