Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kujiendesha kwa faida katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Dkt Ndugulile ametoa pongezi hizo jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha utendaji kazi kilichoshirikisha Mameneja wa TTCL kutoka mikoa yote wa Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na Menejimenti ya Shirika hilo.
Pamoja na mafanikio ya shirika hilo, Dkt Ndugulile ameitaka TTCL kuacha kufanya biashara kwa mazoea bali wawe wabunifu, wafanye utafiti wa soko ili kubaini mahitaji ya wateja wao.

Amesisitiza kila Meneja wa mkoa wa TTCL apewe malengo ya kuongeza wateja, kushughulikia malalamiko ya wateja kwa wakati, kutoa huduma nzuri kwa wateja na kuhakikisha TTCL inakuwa na huduma za kuridhisha.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Waziri Kindamba alimweleza Waziri Ndugulile kuwa shirika hilo limeweza kujiendesha kwa faida kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/2017 kwa kutengeneza faida ya shilingi bilioni tano kwa mwaka, tofauti na miaka ya nyuma ambapo shirika hilo lilikuwa likijiendesha kwa hasara.
