Tozo katika bidhaa za mafuta kupunguzwa

0
4936

Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kupunguzwa  kwa tozo zinazotozwa na Taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta  hapa nchini , zenye thamani ya shilingi bilioni 102 kwa mwaka ili kuwapa unafuu Wananchi.

Rais Samia Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo hayo mkoani Dodoma wakati akipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Nishati, January  Makamba kuhusu utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa wizara hiyo kupitia mwenendo wa biashara ya mafuta na bei zake hapa nchini.

Utekelezaji wa maagizo hayo umeenda pamoja na marekebisho ya kanuni mbalimbali zinazohisu tozo, na yatachapishwa katika gazeti la Serikali leo Oktoba 05 , 2021.

Rais  Samia Suluhu Hassan amefikia uamuzi huo ili kukabiliana na upandaji wa bei za mafuta katika soko la dunia, ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikipanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri watumiaji wa bidhaa hiyo hapa nchini.

Taasisi zinazoguswa na maelekezo ya kupunguzwa kwa tozo hizo ni pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (tozo ya udhibiti), Mamlaka ya Bandari (tozo ya miundombinu), Mamala ya Mapato Tanzania ( tozo ya kuchakata taarifa) na Shirika la Viwango Tanzania ( tozo ya kupima ubora wa mafuta kwenye meli na gharama ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta).

Nyingine ni Wakala wa Vipimo Tanzania (tozo ya uhakiki wa ujazo wa mafuta melini), Wakala wa Usimamizi wa Meli (tozo ya forodha) na Mamlaka ya Serikali  za Mitaa (ushuru wa huduma kwenye halmashauri nne zenye maghala ya kupokea mafuta kwa jumla). 

Halmashauri hizo ni Kigamboni na Temeke za mkoani Dar es Salaam, Tanga pamoja na Mtwara.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza ufanyike mchakato wa haraka wa kupeleka marekebisho ya Sheria Bungeni endapo zipo Sheria nyingine zinazohitaji marekebisho ya haraka katika kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta  hapa nchini.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nishati January Makamba, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu.Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara  Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu.