TIC yatakiwa kuwatembelea Wawekezaji wazawa

0
3344

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Uwekezaji Angela Kairuki, ameuagiza uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutembelea na kugakua mazingira ya Wafanyabiashara na Wawekezaji wazawa waliopo mkoani Ruvuma ndani ya kipindi cha siku Saba.

Waziri Kairuki ametoa agizo hilo alipotembelea kiwanda cha kutengeneza kahawa cha wilaya ya Mbinga cha MCCCO pamoja na kiwanda cha DAE, kwa lengo la kukagua mazingira na utendaji wa viwanda hivyo.

Ametoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa, TIC haijawafikia Wawekezaji wazawa waliopo mikoani, ili kuwatambua na kuwaelimisha kuhusu fursa zinazotolewa na kituo hicho.

 “Ninawaagiza TIC mfike katika viwanda hivi ndani ya siku Saba kuanzia sasa, ili kuwatembelea na kuwaeeleza huduma zinazotolewa na taasisi yenu ikiwemo fursa zilizopo na endapo wataona inafaa wajisajiri kwa kuwa ni suala la hiari,”amesisitiza Waziri Kairuki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa TIC Mafutah Bunini amesema kuwa, katika kuboresha utendaji wao, wamefungua ofisi za Kanda Saba ili kuwafikia kwa urahisi Wawekezaji wa ndani na kwamba wanatoa uzito sawa kwa Wawekezaji wa ndani na wa nje.